Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maeneo matano ya urithi wa dunia Libya hatarini- UNESCO

Maeneo matano ya urithi wa dunia Libya hatarini- UNESCO

Kamati ya urithi wa dunia, leo imeweka maeneo matano ya urithi wa dunia nchini Libya kwenye orodha ya maeneo kama hayo yaliyo hatarini, kufuatia uharibifu uliotokana na mzozo unaoiathiri nchi hiyo, na hatari ya uharibifu zaidi inayotokana na mzozo huo.

Maeneo hayo matano ni maeneo ya akiolojia ya Cyrene, Leptis Magna, Sabratha, eneo la Tadrart Acacus penye sanaa ya mwamba, na mji mkongwe wa Ghadamès.

Kamati hiyo imezingatia hali tete inayoikabili Libya, na kuwepo kwa vikundi vyenye silaha kwenye maeneo hayo, au karibu nayo.

Orodha ya maeneo ya urithi wa dunia yaliyo hatarini imewekwa ili kuifahamisha jamii ya kimataifa kuhusu mazingira yanayotishia sifa zilizoyafanya maeneo hayo kuorodheshwa kama urithi wa dunia, kwa minajili ya kuchagiza uungwaji mkono katika kuyalinda maeneo hayo.