Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban amezitaka Israel na Palestina kutekeleza mapendekezo ya Quartet

Ban amezitaka Israel na Palestina kutekeleza mapendekezo ya Quartet

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon Jumanne amezitaka Palestina na Israel kufanya majadiliano mara moja na chombo cha pande tatu cha kusaka amani ya Mashariki ya Kati Quartet, ili kutekeleza mapendekezo yalitotolewa na chombo hicho hivi karibuni.

Ban amesema lengo ni kumaliza mkwamo wa kisiasa baina ya pande hizo mbili, kuhakikisha utawala wa Palestina kwenye Ukingo wa Magharibi pia kuwa na majadiliano kuhusu masuala yote ya hatima ya suala la mzozo wa Mashariki ya Kati. Akizungumza kwenye kikao cha baraza la usalama hii leo Ban amehoji

(SAUTI BAN 1)

“Ni vipi upanuzi wa makazi ya walowezi , kupokonya ardhi kwa ajili ya matumizi ya Waisrael na kuwanyima Wapalestina maendeleo kuwe ni kukabiliana na ghasia? Sera hizo hazitotimiza ndoto ya kuleta suluhu ya mataifa mawili”

Ameongeza kuwa sera hizo pia hazitohakikisha utulivu na usalama kwa Waisrael bali sera hizo zitaleta hali tofauti. Kisha akawageukia Wapalestina na kusema

(SAUTI BAN CUT 2)

“Wakati huohuo wale Wapalestina wanaosherehekea na kuchagiza mashambulizi dhidi ya watu wasio na hatia ni lazima watambue kwamba hawatekelezi matakwa ya watu wao wala amani. Vitendo hivyo lazima vilaaniwe kimataifa na hatua zaidi zichukuliwe kukabiliana na uchagizaji unaochochea na kuhalalisha ugaidi”