Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi dhidi ya wakimbizi wa ndani na raia Sudan Kusini yanasikitisha:Beyani

Mashambulizi dhidi ya wakimbizi wa ndani na raia Sudan Kusini yanasikitisha:Beyani

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa amesema ameshangazwa na mashambulizi dhidi ya wakimbizi wa ndani na raia wa Sudan Kusini, na ametoa wito wa ukomeshaji wa uhasama. Chaloka Beyani,mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu za wakimbizi wa ndani ametoa taarifa hii leo Jumatatu.

Mapigano yalizuka baina ya vikosi vinavyomuunga mkono Salva Kiir na majeshi ya upinzani ya makamu wake wa kwanza wa Rais Riek Machar Alhamisi iliyopita na kuendelea hadi mwishoni mwa wiki. Zaidi ya watu 10,000 wametawanywa na machafuko hayo wengine zaidi 30,000 ambao tayari walikuwa wakimbizi wa ndani Juba wamefungasha virago.

Wakati huohuo mjini Wau inakadiriwa kwamba watu 83,000 hivi sasa wanapata hifadhi makanisani, mashuleni na nje ya majengo ya kituo cha Umoja wa Mataifa. Bwana Beyani amesema anatambua kwamba wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu wamezuiliwa na kutishiwa katika vituo vya upekuzi walipokuwa wakijaribu kupeleka msaada, na hawawezi kuwafikia watu wanaohitaji msaada.