Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uongozi Sudan Kusini umeshindwa na kuangusha watu wake:Ban

Uongozi Sudan Kusini umeshindwa na kuangusha watu wake:Ban

Mapigano mapya Sudan Kusini yanashtua, kusikitisha na kudhalilsha, na ni pigo lingine katika mchakato wa amani nchini humo.

Hayo ni kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon, amesema machafuko hayo yanaongeza madhila kwa mamilioni ya watu na kukebehi jitihada za kuleta amani ya kudumu.

Mamia ya watu wameuawa na kuna hofu inayoongezeka kwamba watu wengi zaidi watapoteza maisha katika machafuko hayo.

image
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akihutubia waandishi wa habari.(Picha:UM/Mark Garten)
Ban amelaani vikali mauaji ya walinda amani wawili wa Umoja wa Mataifa kutoka China na mfanyakazi mmoja wa kitaifa mjini Juba. Wakimbizi wa ndani wawili pia wamepoteza maisha katika mashambulizi kwenye maskani ya mpango wa Umoja wa Mataifa (UNMISS) na wengine 35 kujeruhiwa. Huku maelfu ya watu wakiendelea kufungasha virago kunusuru maisha yao Ban amesonta kidole kwa viongozi wa taifa hilo changa

(SAUTI YA BAN KI-MOON)

 “Kwa mara nyingine, viongozi wa Sudan Kusini wamewaangusha watu wao, ni nadra kwa nchi kufuja ahadi namna hii na kwa haraka sana. Ni uongozi wa aina gani ambao unaamua kutumia silaha za mauaji na utambulisho wa kisiasa tena na tena?ni uongozi ulioshindwa.”

 

image
Wakimbizi waliofurushwa makwao kufuatia ghasia mpya nchini Sudan Kusini.(Picha:Beatrice Mategwa / UN – South Sudan)
Ban pia ametoa wito kwa nchi wachangiaji wa vikosi kwa UNMISS kushikilia msimamo wao wa kuisaidia Sudan Kusini kwani amesema hatua yoyote ya kuondoka vikosi kwa sasa kutatuma ujumbe usio sahihi kwa Sudan Kusini na kote duniani.
image
Walinda amani wa UNMISS.(Picha:UM/Isaac Billy)
Amesema atakutana na Baraza la Usalama Jumanne mchana kujadili hali hiyo na kusisitiza kwamba huu ni wakati wa kuhimiza hatua za Umoja wa Mataifa. Wakati nchi inashindwa au itashindwa kulinda watu wake, na pale ambapo pande kinzani zinajihami na kujiwezesha kwa dhamana ya watu wake, basi jumuiya ya kimataifa ina wajibu wa kuchukua hatua.

Hivyo amelitaka Baraza la Usalama na wanachama wote wa Umoja wa Mataifa kusimama kidete wakati huu na kulinda haki za binadamu za watu wa Sudan Kusini. Katika maswali na majibu Ban amesema anatumai miongoni mwa hatua Baraza la Usalama iliiwekee sudan Kusini vikwazo vikiwemo vya silaha.