Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la usalama: mapigano Sudan Kusini yakome, nchi zijiandae kutuma vikosi zaidi

Baraza la usalama: mapigano Sudan Kusini yakome, nchi zijiandae kutuma vikosi zaidi

Wajumbe wa baraza la usalama wamelaani vikali mapigano mapya yaliyozuka na kuendelea Juba Sudan Kusini. Katika kikao maalumu Jumapili wajumbe hao pia wameelezea kushtushwa na kukasirishwa na mashambulizi kwenye maskani ya Umoja wa Mataifa na yanayotoa ulinzi wa raia Juba.

Wajumbe wa baraza wametaka machafuko hayo yaliyoanza tarehe 7 mwezi huu kukoma mara moja kwa pande zote na wamemtaka Rais Salva Kiir na makamu wa kwanza wa Rais Riek Machar kufanya kila liwezekanalo kudhibiti vikosi vyao, kukomesha mapigano haraka , kuzuia kuenea kwa machafuko na kujidhatiti kutekeleza mkataba wa amani mara moja ikiwa ni pamoja kukomesha uhasama na kuondoa vikosi vyao Juba.

Wajumbe wamezichagiza nchi katika kanda hiyo, baraza la amani na usalama la Muungano wa Afrika na mamlaka ya maendeleo ya kikanda IGAD , kuendelea kushirikiana na viongozi wa Sudan Kusini kushughulikia mzozo huo.

Baraza pia limesisitiza msaada wake kwa mpango wa Umoja wa mataifa Sudan Kusini UNMISS, na limeelezea nia ya kutaka kuimarisha mpango huo ili kuhakikisha kwamba UNMISS na jumuiya ya kimataifa wanaweza kuzuia na kukabiliana na ghasia Sudan Kusini.

Limezichagiza pia nchi katika kanda kujiandaa kutoa vikosi vya ziada endapo baraza litaamua hivyo, lakini kwa sasa baraza limesisistiza haja ya UNMISS kutumia mamlaka yake na kutimia kiloa njia kuwalinda raia.