Wanasiasa Sudan Kusini onyesheni uongozi imara:UM

Wanasiasa Sudan Kusini onyesheni uongozi imara:UM

Kukiwa na machafuko mapya Sudani Kusini duru zikisema yamekatili maisha ya watu 150, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limeitaka serikali ya Sudan Kusini kuonyesha uongozi imara na kurejea katika lengo la kuleta amani ya kudumu.

Taifa hilo changa kabisa duniani limesherehekea miaka mitano ya uhuru Jumamosi wiki hii , huku mapigano yakiendelea baina ya serikali na wanajeshi wa upinzani katika mji mkuu Juba.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema ameshitushwa na kusikitishwa na mapiganop hayo mazito na kusema katika taarifa yake kwamba maskani ya Umoja wa Mataifa na maeneo yanayohifadhi na kulinda raia pia yamekubwa na machafuko hayo.

Ameongeza kuwa amefadhaishwa na kuzuka upya kwa mapigano. Taarifa ya baraza la usalama nayo imelaani vikali mapigano hayo .Baraza limesema mapigano yameendelea mwishoni mwa wiki licha ya wito kutolewa na Rais Salva Kiir na makamu wa pili wa Rais Riek Macher kutaka kurejeshwa kwa utulivu.

Viongozi hao wawili walitia saini mkataba wa amani karibu mwaka mmoja uliopita , baada ya miaka kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Baraza la usalama limesema linatiwa hofu na pande hizo mbili kutoonyesha kujidhatiti kwao katika kutekeleza mkataba wa amani na kuonya kwamba endapo mapigano yataendelea hatua nzaidi zitachukuliwa kwa kuzingatia maazimio ya baraza la usalama.

Taarifa imesisitiza umuhimu wa vikosi vya jeshi kuwajibishwa kwa vitendo vyao, na limeitaka serikli kufanya uchunguzi wa kina , huku likiziasa pande zote katika mzozo kuruhusu mpango wa Umoja wa mataifa nchini humo UNMISS kufikisha msaada muhimu wa kibinadamu unaohitajika na kuwalinda raia waliojikuta katikati ya mapigano.