Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano yaibuka Juba, Ban asema ni ulaghai kwa wananchi wa Sudan Kusini

Mapigano yaibuka Juba, Ban asema ni ulaghai kwa wananchi wa Sudan Kusini

Mapigano yameripotiwa huko Juba, Sudan Kusini kati ya wanajeshi wa Sudan People’s Liberation Army, SPLA na wale waliojitenga kutoka kikundi hicho, SPLA-O.

Kufuatia ripoti za kuendelea kwa mapigano hayo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema ana wasiwasi mkubwa wakati huu ambao ni mkesha wa nchi hiyo kuadhimisha miaka mitano tangu kupata uhuru kutoka Sudan.

Ban kupitia msemaji wake amesema mapigano hayo ni kiashiria ya jinsi ambavyo pande husika kwenye mzozo hazina utayari wa dhati kutekeleza makubaliano ya amani.

Amesema hali hiyo ni ulaghai mpya kwa wananchi wa Sudan Kusini ambao wamekuwa wakikumbwa na hali ngumu tangu kuibuka kwa mzozo Disemba 2013.

Ban amegusia pia mapigano yaliyoibuka huko Wau na Bentiu, akisema yanaweza kuzorotesha usalama nchini kote.

Amewasihi rais Salva Kiir na makamu wa kwanza wa rais Riek Machar kumaliza mapigano yanayoendelea na kuwachukulia hatua viongozi wa kijeshi waliohusika na kuanza kwa mapigano hayo ili hatimaye mkataba wa amani utekelezwe.

Katibu Mkuu amesema Umoja  wa Mataifa kwa upande wake unasalia na Sudan Kusini na pande zote zinazosaidia nchi hiyo kurejea katika amani na utulivu.