Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madhila ya watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu nchini Burundi

Madhila ya watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu nchini Burundi

Usaidizi kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu ni moja ya jukumu la Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la kuhudumia watoto UNICEF na wadau wengine ikiwemo nchi wanachama na asasi za kiraia.

Barani Afrika husuani Afrika Mashariki Watoto hawa hufahamika zaidi kama watoto wa mitaani ikibeba tafsiri ya watoto wasio na mwenyewe yaani wazazi, walezi au jamii na mamlaka za nchi zimewatelekeza na hivyo kuishia kuishi mitaani.

Wengi wao hujikuta wakitumbukia kwenye ajira za utotoni ambazo ni kosa kwa mujibu wa sheria za kitaifa na kimataifa ikiwemo mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto, CRC.

Kwa mujibu wa mkataba huo unaotambua mtu yeyote mwenye umri wa chini ya miaka 18 ni mtoto, kundi hili halipaswi kubaguliwa kwa misingi yoyote ile ikiwemo rangi, dini, aina ya familia wanazotoka, wanachokisema au kufikiri.

Mkataba huo pia unakwenda mbali zaidi kwa kuwataka watu wazima kulinda maslahi ya watoto lakini pia mamlaka za nchi kulinda haki zao kama vile elimu,  afya, kucheza na mengineyo.

Bara la Afrika kwa kutambua wajibu huo huadhimisha siku ya mtoto wa Afrika kila Juni 16 ili kuangazia jukumu la kusaidia kundi hili.

Burundi ni miongoni mwa nchi zilizoadhimisha siku hii ambako mwandishi wetu wa maziwa makuu Ramadhani Kibuga alivinjari jijini Bujumbura kushuhudia watoto wanaoshi katika  mazingira magumu.