Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 250,00 kufa kila mwaka kutokana maradhi yanayoambatana na mabadiliko ya nchi :WHO

Watu 250,00 kufa kila mwaka kutokana maradhi yanayoambatana na mabadiliko ya nchi :WHO

Washiriki katika mkutano wa kimataifa wa pili kuhusu afya na tabia nchi , ulioandaliwa na serikali ya Ufaransa Rais wa mkutano wa COP21 , wamependekeza hatua za utekelezaji wa makubaliano ya mkataba wa Paris ili kupunguza hatari za afya zinazohusiana na mabadiliko ya tabia nchi.

Ajenda hiyo ya hatua ni mchango wa COP22 , chini ya Urais wa serikali ya Morocco, kwani mkutano huo wa COP22 utafanyika Marrakech mwezi Novemba 2016.

Shirika la afya ulimwenguni WHO linakadiria kuwa mabadiliko ya tabia nchi tayari yanasababisha maelfu ya vifo kila mwaka.

Vifo vinavyoongezeka mara kwa mara kutokana na maradhi kama kipindupindu, maradhi mengine ya jiografia kama homa ya kidingapopo na wengine kupoteza maisha kutokana na hali ya hewa kama joto la kupundukia na mafuriko.

Wakati huohuo WHO imesema takribani watu milioni 7 hufa kila mwaka kutokana na maradhi yanayosababishwa na uchafuzi wa hali ya hewa yakijumuisha saratani na kiarusi.

Wataalamu wanakadiria kwamba ifikapo mwaka 2030, mabadiliko ya hali ya hewa yatasababisha ongezeko la vifo 250,000 kila mwaka kutokana na kuhara, shikikizo la moyo, ukosefu wa lishe pekee.Na waathirika wakubwa watakuwa watoto, wanawake, wazee na masikini.