Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuelekea miaka mitano ya uhuru Sudan Kusini, raia wengi bado wakimbizi- UNHCR

Kuelekea miaka mitano ya uhuru Sudan Kusini, raia wengi bado wakimbizi- UNHCR

Wakati Sudan Kusini ikielekea kaudhimisha miaka mitano ya uhuru wake tarehe tisa mwezi huu, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesalia na wasiwasi mkubwa juu ghasia zinazoendelea nchini humo na kusababisha watu kukimbia makazi yao hata kwenda nchi za jirani.

Taifa hilo changa zaidi duniani linaongoza duniani kwa kuwa na wakimbizi watokanao na mizozo ambapo raia mmoja kati ya wanne ni mkimbizi wa ndani au nchi jirani.

UNHCR inasema raia ndio wanabeba mzigo mkubwa wa mzozo uliozuka Disemba 2013, uhakika wa chakula ukisalia ndoto na usaidizi wa kibinadamu nao ukisuasua.

Melissa Fleming ni msemaji wa UNHCR, Geneva, Uswisi.

“Licha ya makubaliano ya amani yaliyokomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe mwezi Agosti mwaka jana, mzozo na ukosefu wa utulivu vimeenea kwenye maeneo ambayo awali yalikuwa na utulivu. Halikadhalika hakuna kiwango kikubwa cha wakimbizi wanaorejea nyumbani.”

Nao ujumbe wa Mataifa nchini Sudan Kusini umelaani vikali kuzuka kwa ghasia hivi karibuni huko Wau, Juba na Bentiu, kulikosababisha vifo na majeruhi miongoni mwa raia.