Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban asihi China iachie makundi ya kiraia yafanye kazi zao

Ban asihi China iachie makundi ya kiraia yafanye kazi zao

Katibu Mkuu wa Umoja wa Matifa Ban Ki-moon yuko China kwa ziara ya siku tano ambako amekuwa na mazungumzo na viongozi mbali mbali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje Wang Yi.

Wawili hao wamejadili masuala kadhaa ya kimataifa na kikanda ikiwemo mvutano katika rasi ya Korea ambapo Ban amesema Umoja wa Mataifa una wasiwasi mkubwa juu ya hali inayoendelea.

Halikadhalika ametumia fursa hiyo kutoa pole kwa vifo vilivyotokana na mafuriko kwenye majimbo kadhaa nchini China sambamba na uharibifu wa mali.

Baada ya mazungumzo kati yao, walizungumza na waandishi wa habari ambapo Katibu Mkuu ametumia fursa hiyo kuzungumzia kubinywa kwa wanaharakati nchini China ambapo amesema..

(Sauti ya Ban)

"Nahamasisha mamlaka za China ziweke fursa zinazohitajika kwa mashirika ya kiraia kutekeleza majukumu yao adhimu. Wanaharakati wa mazingira, wanasheria na watetezi wa haki za binadamu, wafuatiliaji wa utawala bora wa serikali na makundi mengine ya kiraia yanaweza kuchagiza maendeleo ya kijamii na ukuaji wa kiuchumi. Wanaweza kuwakilisha maslahi tofauti ya jamii na kuleta sauti za walio pembezoni.”.