Milioni 15.5 kupatiwa chanjo dhidi ya homa ya manjano Angola na DRC

Milioni 15.5 kupatiwa chanjo dhidi ya homa ya manjano Angola na DRC

Shirika la afya ulimwenguni, WHO kwa kushirikiana na serikali za Angola na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC watapatia chanjo watu Milioni 15 na nusu dhidi ya homa ya manjano. Joseph Msami na ripoti kamili.

(Taarifa ya Msami)

Homa ya manjano imekuwa tishio siyo tu Angola bali pia DRC ambapo, Mkurugenzi Msaidizi wa WHO anayehusika na dharura za magonjwa Dkt. Bruce Aylward amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kuwa kampeni hiyo itaanzia mwezi huu wa Julai hadi Agosti msimu wa mvua utakapokuwa umekamilika. Kampeni itafanywa kwa ushirikiano na serikali.

(Sauti Bruce)

"Kwa hiyo kampeni itakuwa watu milioni Nane Kinshasa, takribani watu Milioni Tatu mpakani mwa DRC, na wengine milioni moja na nusu upande wa mpaka na Angola na wengine milioni Tatu nchini Angola ambako bado kuna masalia ya maambukizi ya ugonjwa.”

Kwa mujibu wa WHO, homa ya manjano licha ya kuwa na chanjo bado imesalia katika nchi 47 duniani ambako 33 kati yao ziko Afrika.