Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

El Niño yatokomea lakini yaacha madhara makubwa kwa watoto

El Niño yatokomea lakini yaacha madhara makubwa kwa watoto

Msimu wa El Niño kwa mwaka 2015-2016 umemalizika, lakini madhara yake kwa watoto yanazidi kuongezeka.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF ikiongeza kuwa njaa, utapiamlo na magonjwa vinaendelea kuongezeka kufuatia ukame mkali na mafuriko yaliyotokana na hali hiyo ya hewa.

Mathalani uhaba wa chakula unakwamisha matumizi ya dawa za kupunguza makali ya Ukimwi, ripoti ikiongeza kuwa iwapo La Niña itakuwepo baadaye mwaka huu, hali ya kibinadamu itazidi kuwa mbaya.

Mkurugenzi wa UNICEF anayehusika na masuala ya dharura wa Afshan Khan amesema maeneo ya mashariki na kusini mwa Afrika yameathirika zaidi, watoto Milioni 26 na nusu wakihitaji msaada.

UNICEF imetoa wito kwa serikali kuimarisha mipango ya kuhimili majanga ikiwemo yale yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi.