Skip to main content

Wakimbizi wengi zaidi wa Syria wanaishi katika umasikini:UNHCR

Wakimbizi wengi zaidi wa Syria wanaishi katika umasikini:UNHCR

Wakimbizi wa Syria wanaishiwa na akiba baada ya miaka mitano ya vita na wengi wao wanaishi katika umasikini kuliko wakati mwingine wowote.

Hii ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, ambalo pamoja na washirika wake wametoa ripoti kuhusu hali ya wakimbizi Uturuki, Jordan, Iraq, Lebanon na Misri.

Kwa pamoja nchi hizi zinahifadhi wakimbizi wa Syria milioni 4.8. Nchini Lebanon asilimia 70 ya wakimbizi sasa wanaishi katika ufukara ikiwa ni ongezeko la asilimia 50 ikilinganishwa na 2014.

Ripoti hiyo pia inaainisha kwamba nchi zinazohifadhi watu wanaokimbia Syria zinakabiliwa na shinikizo kubwa ya kuwapa hata huduma za msingi kwa wale wanaozihitaji.

Ugumu wa kuwapatia msaada wanaouhitaji umeongezwa na ukosefu wa ufadhili. Na hii ni licha ya ahadi zilizotolewa mapema mwaka huu mjini London kwenye mkutano kwa ajili ya Syria, na hadi sasa ni asilimia 30 tuu ya ahadi hizo ndio imelipwa.