Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO, FAO waendesha mafunzo kwa wafugaji Sudan Kusini

UNESCO, FAO waendesha mafunzo kwa wafugaji Sudan Kusini

Kwa mara ya kwanza katika historia ya maisha yao, wakulima katika ukanda Ziwa nchini Sudan Kusini wamehudhuria darasa la kuwa wakufunzi wa jamii na kujihisi wamekaa muda mrefu na mazizi ya mifugo yao.

Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO, lile la chakula na kilimo FAO kwa kuishirikiana na wadau, wanaendesha mradi wa kuwawezesha kimaarifa na elimu wafugaji nchini humo ili wakabiliane na kudorora kwa ustawi wao.

Kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya EU, na usaidizi wa wizara za serikali ya Sudan Kusini mradi unawalenga watoto, vijana na watu wazima katika maeneo ambayo yana ukosefu wa fursa za elimu , migogoro , ukosefu wa chakula , ajira na wizi wa mifugo.

Mradi huu umeleta mafanikio makubwa kwa wakulima mathalani Michael ambaye amekiri kuwa anakumbuka kila alichofundishwa ikiwamo ishara na dalili za mnyama mgonjwa na kadhalika anaeleza namna alivyonufaika na mafunzo ya namna ya kuendeleza wazo la biashara.

Michael ambaye sasa ni mkufunzi wa kambi ya wakulima baada ya kurejea nyumbani amepewa siku za mapumziko na huenda airejelee tena kazi yake ya awali ya kuchunga mifugo kwakuwa atakuwa mkufunzi. Tayari ameanza kuwafunza nduguze na majirani.