Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Israeli kujenga makazi zaidi, Ban asema ni kinyume cha sheria

Israeli kujenga makazi zaidi, Ban asema ni kinyume cha sheria

Uamuzi wa mamlaka za Israel kuendelea na mipango yake ya kujenga takribani makazi 560 kwenye ukingo wa magharibi wa mto Jordan na makazi 240 Yerusalem Mashariki umelaaniwa vikali na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon.

Katika taarifa kupitia msemaji wake, Ban amesema hatua hiyo inaibua hoja ya mipango ya muda mrefu ya Israel inayosongeshwa na kauli za mara kwa mara za mawaziri wa Israeli za kujiongezea eneo la Ukingo wa magharibi wa mto Jordan.

Ban amesisitiza kuwa uamuzi wa sasa ni kinyume na sheria ya kimataifa na amesihi serikali ya Israel kusitisha na kubadili uamuzi huo kwa maslahi ya amani na kuwa na kuhitimisha makubaliano yenye haki.

Katibu Mkuu amesema kinachomsikitisha zaidi, uamuzi wa sasa umekuja siku nne tu baada ya mpango wa pande nne, au Quartet kuhusu Mashariki ya Kati uliotoa wito kwa Israeli kusitisha sera zake za ujenzi wa makazi ya walowezi na kujitwalia maeneo.