Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban aguswa na kifo cha mpaza sauti dhidi ya mauaji ya kimbari, Elie Wiesel

Ban aguswa na kifo cha mpaza sauti dhidi ya mauaji ya kimbari, Elie Wiesel

Kufuatia kifo cha Elie Wiesel, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel aliyepaza sauti dhidi ya chuki kwa wayahudi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameeleza kushtushwa kwake na taarifa za kifo hicho.

Ban kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake amesema hayati Wiesel, wakati wa uhai wake alikuwa sauti thabiti kwa kumbukizi ya mauaji ya kimbari ya wayahudi na alikuwa mjumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa kwa muda mrefu.

Elie Wiesel ambaye amefariki dunia Jumamosi nchini Marekani akiwa na umri wa miaka 87, alitumia ujana wake kuanzisha kampeni ya kudumu ya kusaka usawa na amani.

Akiwa mjumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa tangu mwaka 1998, Wiesel alitoa wito mara kwa mara wa kukomeshwa kwa chuki dhidi ya wayahudi na aina nyinginezo za chuki.

Ban amesema mara kwa mara alifika Umoja wa Mataifa ikiwemo wakati wa maadhimisho ya kwanza kabisa ya siku ya kimataifa ya kumbukizi ya wahanga wa mauaji ya kimbari ya wayahudi akielezea pia uzoefu wake katika kambi ya Auschwitz Birkenau ambayo manazi wa Ujerumani walitumia kwa ajili ya mateso na kuteketeza wayahudi.

Katika Mkuu ametuma rambirambi zake kwa mjane wa Wiesel, familia na wale wote walioguswa na kifo chake, akisema Umoja wa Mataifa unashukuru sana kwa mchango wa Wiesel na utaendelea kusimama kidete kwa kumbukizi na kusaka haki za binadamu kwa wote.