Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Marekani imetangaza msaada wa dola milioni $52 zaidi kwa wakimbizi wa Palestina

Marekani imetangaza msaada wa dola milioni $52 zaidi kwa wakimbizi wa Palestina

Ufadhili wa ziada kwa wakimbizi wa Palestina wa jumla ya dola milioni 51.6 umetangazwa na serikali ya Marekani Alhamisi ili kukidhi ombi la msaada wa dharura lililotolewa.

Shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Palestina UNRWA lilitoa ombi la msaada wa dharura ili kusaidia kazi zake katika maeneo ya Wapalestina yanayokaliwa.

Msaada huu umekuja kipindi muhimu na muafaka kabisa wakati mahitaji ya dharura yakiongezeka amesema afisa wa UNRWA Sandra Mitchell.

Akitoa tangazo hilo kwenye kambi ya wakimbizi kwenye Ukingo wa Magharibi mjini Bethlehem, afisa wa ubalozi wa Marekanil Donald Blome, amesema nchi yake inajinasibu kwa jukumu lao la kuwa msitari wa mbele katika ufadhili.

UNRWA inasema msaada huo utatumika kuboresha maisha ya watu, afya ya akili katika jamii, ulinzi na usalama, pamoja na msaada wa dharura wa chakula, vituo vya afya na elimu.