Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Burundi ichukue hatua zaidi kulinda haki za binadamu- Zeid

Burundi ichukue hatua zaidi kulinda haki za binadamu- Zeid

Huko Geneva, Uswisi, kamishna mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad al Hussein amewasilisha ripoti kuhusu ushirikiano wa kiufundi na ujenzi wa uwezo wa Burundi katika kuimarisha haki za binadamu.

Zeid akizungumza mbele ya baraza la haki za binadamu, pamoja na mambo mengine ameelezea kuzorota kwa hali ya haki za binadamu ikiwemo wageni kukumbwa na misukosuko wanapoingia Burundi kwa madai kuwa wanaweza kujiunga na vikundi vya waasi.

Hata hivyo ametaja hatua chanya za serikali za kurejesha hali ya utulivu ikiwemo kufuta hati za kimataifa za kukamatwa kwa wafuasi wa mashirika ya kiraia na vyama vya upinzani, huku akitoa wito kwa serikali..

(Sauti)

Nasihi kukomeshwa kwa ukiukwaji wa haki za binadamu unaotokomeza maisha, matarajio na mustakhbali wa wananchi na taifa, na kusaka suluhu ya mzozo huu kupitia mashauriano ya dhati ya kitaifa ambayo ni shirikishi.”

Kwa upande wake waziri wa jamii na jinsia wa Burundi Martin Nivyabandi akizungumza mbela ya baraza la haki za binadamu amedai kuwa ripoti hiyo imekuwa kimya katika mambo yaliyotokea nchini humo kabla ya Aprili 2015 kwa madai kuwa baadhi ya watu walitaka kupindua nchi.