Baraza la Haki za Binadamu lamulika michezo na haki za binadamu
Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, leo limekuwa na majadaliano kuhusu matumizi ya michezo na maadili ya Olimpiki katika kuendeleza haki za binadamu kwa wote.
Akizungumza katika mjadala huo, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Zeid Ra’ad Al Hussein, amesema kuwa michezo inaweza kuwa nguvu thabiti ya kuleta usawa na kuheshimiana kwa watu wenye asili mbalimbali, akitaja kuwa wanariadha 10 watashiriki katika michezo ya Olimpiki mwaka huu wa 2016 kama timu ya wakimbizi.
Kamishna Zeid amesema ushiriki wa wanariadha hao wakimbizi huenda ukahamasisha uelewa mpya kuhusu haki za mamilioni ya watu walionaswa katika mizozo duniani, na ambao kilicho muhimu zaidi kwao siyo medali wala sifa, bali ni haki ya kuwa hai, usalama na utu wao.