Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto masikini wakabiliwa na hatari ya ujinga na vifo vya mapema

Watoto masikini wakabiliwa na hatari ya ujinga na vifo vya mapema

Kutokana na mwelekeo wa sasa, watoto milioni 69 watafariki dunia kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika, huku watoto milioni 167 wakiishi katika umaskini, iwapo dunia haitamulika zaidi hatma ya watoto maskini.Taarifa kamili na John kibego.

(Taarifa ya Kibego)

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya Shirika la Kuhudumia Watoto (UNICEF), ambayo pia imesema wanawake milioni 750 watakuwa wameolewa wakiwa bado watoto ifikapo mwaka 2030, lakini kufanya uamuzi mwafaka sasa kunaweza kubadili mwelekeo huo.

Ripoti hiyo ya kila mwaka inaweka picha ya kutia hofu kuhusu hatma ya watoto masikini zaidi, iwapo jamii ya kimataifa haitoongeza kasi ya kushughulikia mahitaji yao.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Anthony Lake, amesema kuwanyima mamia ya mamilioni ya watoto fursa maishani siyo tu kunatishia mustakhbali wao, bali pia kunachochea mzunguko wa umaskini na taabu katika vizazi vijavyo.