Skip to main content

Mafanikio ya Somalia katika masuala ya haki yamulikwa Geneva

Mafanikio ya Somalia katika masuala ya haki yamulikwa Geneva

Baraza la Haki za Binadamu limekutana leo kwa ajili ya kuzungumzia tathmini ya mara kwa mara ya Somalia, nchi wanachama zikipongeza nchi hiyo kwa jitihada katika kuendeleza haki za wanawake.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imeeleza kwamba nchi wanachama zilizohudhuria mkutano huo zimemulika mafanikio yaliyopatikana nchini Somalia katika kuimarisha ulinzi wa haki za binadamu, uwezeshaji wa wanawake na haki za watoto.

Akihutubia mkutano huo, Mwakilishi wa kudumu wa Somalia kwenye ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva Uswisi, Faduma Abdullahi Mohamud amesisitiza kwamba Somalia inajaribu kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa na Ofisi ya Haki za Binadamu, pamoja na kwamba rasimali ya nchi hiyo ni duni. Aidha ametangaza kwamba Bunge la Somalia hivi karibuni limepitisha sheria ya kuunda Tume huru ya Haki za Binadamu. Halikadhalika, amesema serikali imepitisha mpango maalum wa kuongeza ushiriki wa wanawake kwenye jukwa la siasa.

Kwa upande wao, taasisi zisizo za kiserikali zimemulika hali ya usalama wakisema bado kundi la Al-Shabaab linatawala eneo kubwa la nchi. Aidha wamesema bado uhuru wa vyombo vya habari haujathibitishwa, huku ukwepaji sheria ukiwa unaendelea hasa katika uongozi wa jeshi.