Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali ya Colombia na FARC wasaini makubaliano muhimu

Serikali ya Colombia na FARC wasaini makubaliano muhimu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema kutiwa saini kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya serikali ya Colombia na waasi wa FARC-EP ni hatua ya kihistoria na kwa kuwa ni ishara ya kumalizika kwa mzozo uliodumu muda mrefu zaidi barani Amerika ya Kusini.

Ban amesema hayo huko Havana, Cuba baada ya kushuhudia pande mbili hizo zikifikia hatua hiyo akisema kuwa..

Hii leo mchakato wa amani wa Colombia unahalalisha uvumilivu wa wale wote ulimwenguni ambao wanahaha kumaliza mizozo si kwa njia ya kumsambaratisha adui, bali kupitia uvumilivu na kusaka kulegeza misimamo.”

Katibu Mkuu amepongeza pande zote za mashauriano ambazo amesema zimeonyesha kiwango cha juu cha kusaka amani kwa kuzingatia utu wa pande zote ambapo wamepitia changamoto kubwa, akiongeza kuwa changamoto bado zinasalia na kwamba..

Kutiwa saini kwa sehemu hii muhimu ya makubaliano ya amani kutaimarisha azma hii. Itakuwa muhimu sasa kuhamasisha watu na kufuatialia na kuthibitisha utekelezaji wake.”

Miezi sita iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na jumuiya ya nchi za Amerika ya Kusini, waliitikia wito kutoka serikali ya Colombia na waasi wa FARC-EP na kuazimia kusaidia utekelezaji wa mpango wa amani na kusalimisha silaha.