Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

O’Brien ataka hatua kuhusu hali ya kibinadamu nchini Syria

O’Brien ataka hatua kuhusu hali ya kibinadamu nchini Syria

Mkuu wa Ofisi ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura katika Umoja wa Mataifa (OCHA), Stephen O’Brien, amesema leo kuwa ulimwengu unaendelea kutizama tu, huku Syria ikiendelea kusambaratika kwa umwagaji damu, na kutoa wito hatua zichukuliwe mara moja kukomesha hali mbaya ya kibinadamu nchini humo.

Bwana O’Brien amesema hayo wakati akihutubia wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambao wamekutana kufanya mashauriano kuhusu hali Mashariki ya Kati, wakimulika hasa hali nchini Syria.

Mkuu huyo wa OCHA amesema, katika maeneo mengi ya Syria, machafuko yanaendelea, huku pande kinzani zikiwa zimeshindwa kuelewa kuwa hapawezi kuwepo suluhu ya kijeshi kwa mzozo huo.

Makazi ya raia yanashambuliwa. Vituo vya afya na matibabu vinaharibiwa. Elimu imevurugika, na wanavyotegemea raia kuishi vimeharibiwa. Je, kila mmoja wenu asingetaka kuikimbia hali kama hii pia?"

Bwana O’Brien amesema kuna walakin mkubwa katika dunia inayonyamaza tu pale hospitali, shule, misikiti, masoko, na vikundi vya kidini vinaposhambuliwa, akihoji:

Ni kwa kipindi gani zaidi watoto wa Syria watateseka hivi? Ni kwa muda gani zaidi tutavumilia kutoheshimiwa kabisa kwa kanuni za msingi za ubinadamu- kutoheshimu kabisa sheria ya kimataifa n ahata maazimio ya Baraza hili?”

Awali, Bwana O’Brien amesema anaitoa ripoti hiyo kwa heshima ya Jo Cox, mbunge wa Uingereza aliyeuawa wiki iliyopita kwa misingi ya kupigania umoja badala ya utengano, akisema mbunge huyo alikuwa anapigania pia amani nchini Syria.