Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wajane mara nyingi hunyanyapaliwa na familia na jamii:Ban

Wajane mara nyingi hunyanyapaliwa na familia na jamii:Ban

Kuna takribani wajane milioni 259 duniani kote na karibu nusu wanaishi katika hali ya umasikini.

Katika ujumbe wake kuhusu siku ya kimataifa ya wajane, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema mara nyingi wajane wananyanyapaliwa na familia zao na jamii, huku wengi wakikumbwa na ubaguzi kwa sababu ya umri na jinsia.

Ameongeza kuwa baadhi ya wajane wanaishi maisha yaliyoghubikwa na ukatili wa kimwili na kingono. Wajane wazee wana rasilimali kidogo sana za kiuchumi baada ya maisha yao yote kufanya kazi ngumu ya bila malipo. Na hata katika nchi zilizoendelea Ban amesema thamani ya malipo ya uzeeni kwa wanawake inaweza kuwa asilimia 40 chini ya ile ya wanaume.

Na kwa upande wa wajane wadogo amesema wanakabiliwa na changamoto nyingi, kama vichwa vya familia, huku wakibeba majukumu ya ulezi wa watoto wakiwa na fursa chache sana za kiuchumi.

Wakati ajenda ya maendeleo endelevu ya 2030 ikiahidi kutomwacha yeyote nyuma, Ban amesema wajane wana fursa kama miongoni mwa makundi yanayotengwa na yasiyojiweza.

Katika siku hii ametoa wito wa kuwaenzi wajane katika jamii na kuwasaidia kuishi maisha bora ya uzalishaji, usawa na yanayojitosheleza.