Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mazungumzo ya Syria hayajafutwa kabisa mwezi Julai:De Mistura

Mazungumzo ya Syria hayajafutwa kabisa mwezi Julai:De Mistura

Mazungumzo mapya kuamua hatima ya Syria yanahitajika haraka, na lengo ni kuwezesha kufanyika mwezi Julai amesema Alhamisi mwakilishi maalumu wa Umoja wa mataifa kwa ajili ya Syria Staffan de Mistura.

Akizungumza Geneva, mpatanishi huyo mwenye uzoefu amesema, ataliomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa muongozo katika siku chache zijazo.

Lakini amesisitiza kwamba mafanikio ya mazungumzo ya amani yanategemea shinikizo kutoka kwa Urusi na Marekani.

(SAUTI YA DE MISTURA)

“Msisahau, usitishaji wa uhasama ulifanyika wakati Urusi na Marekani walipoafikiana kuhusu kitu fulani. Na hilo lilileta manufaa. Tunasaka manufaa muhimu kama hayo katika mwanzo wa mpito wa kisiasa. Na tunaweza kusaidia,  lakini tunahitaji hilo”

Ameongeza kuwa fursa ya mazungumzo ya amani kuanza tena inategemea misaada zaidi ya kibinadamu kuwafikia watu kwenye maeneo yanayozingirwa Syria na kuwa na ukiukaji mdogo wa makubaliano ya kusitisha uhasama yaliyoanza Februari.