Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Adama Dieng atiwa wasiwasi na hali Bahrain

Adama Dieng atiwa wasiwasi na hali Bahrain

Mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari, Adama Dieng, ameeleza wasiwasi wake kuhusu uamuzi wa Wizara ya masuala ya ndani nchini Bahrain kutengua uraia wa kiongozi mashuhuri wa imani ya Kishia, na athari za uamuzi huo.

Katika taarifa iliyotolewa leo, Bwana Dieng amesema anafahamu kuwa uamuzi wa kutengua uraia wa Sheikh Issa Qassem umezua maandamano mapya, ambayo anahofia kuwa huenda yakaongeza mivutano nchini Bahrain katika siku chache zijazo.

Mshauri huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa serikali ya Bahrain ihakikishe kuwa uhuru wa watu kujumuika kwa amani unaheshimiwa kikamilifu, na kuwa udhibiti wa maandamano unafanyika kwa misingi ya wajibu wa Bahrain chini ya sheria ya kimataifa ya haki za binadamu.

Halikadhalika, ametoa wito kwa wanaoandamana wafurahie haki zao kwa amani, pamoja na kujiepusha na vitendo vyovyote vya ghasia.