Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada wa fedha kwa wakimbizi Rwanda wainua uchumi wa jamii:WFP

Msaada wa fedha kwa wakimbizi Rwanda wainua uchumi wa jamii:WFP

Utafiti mpya uliofanyika nchini Rwanda umebaini kuwa msaada wa kibinadamu kwa wakimbizi una matokeo mazuri ya kuchumi katika jamii zinazowazunguka, na matokeo yanakuwa bora zaidi pale wakimbizi wanapopewa fedha taslimu badala ya mgao wa chakula, ili kukidhi mahitaji yao ya chakula ya kila mwezi. Taarifa zaidi na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Utafiti huo umefanywa na jopo la watafiti kutoka shirika la Umoja wa mataifa la mpango wa chakula WFP na chuo kikuu cha California, Davis.

Utafiti ulijikita katika kupima matokeo katika jamii ya msaada wa chakula unaotolewa na WFP kwa wakimbizi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC wanaoishi kwenye kambi tatu nchini Rwanda.

Watafiti wametumia mahojiano ya mamia ya wakimbizi, wanajamii wa Kinyarwanda, na wafanya biashara, na kulinganisha takwimu kati ya wakimbizi makambini wanaopokea fedha taslimu na wanaopokea mgao wa chakula wa kila mwezi. Na matokeo ni kwamba wanajamii wanaona faida kubwa za kiuchumi kwa kuhifadhi wakimbizi, na hasa wanaopewa fedha badala ya chakula.