Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tumeanza kuchukua hatua kulinda haki za binadamu- Sudan Kusini

Tumeanza kuchukua hatua kulinda haki za binadamu- Sudan Kusini

Baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na mashauriano kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Sudan Kusini likiangazia pia hatua zilizochukuliwa na serikali kuhakikisha uwajibikaji kwa wale wanaokiuka haki hizo. Taarifa kamili na Flora Nducha.

(Taarifa ya Flora)

Akizungumza kwenye kikao hicho,Naibu Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Kate Gilmore amesema miaka miwili na nusu tangu kuanza kwa mzozo Sudan Kusini hali bado si shwari na hakuna ushahidi dhahiri kwa serikali na upinzani kuchunguza, kufungua mashtaka na kuadhibu wakiukao haki za binadamu.

(Sauti ya Kate)

"Bila hatua hizo, amani ya kudumu Sudan Kusini itasalia ndoto na kuleta madhara makubwa kwa wananchi. Baraza la haki za binadamu liendelee kufuatilia kwa makini ili wahusika wawajibishwe."

Hata hivyo Akech Chol Ahou, mwakilishi wa Sudan Kusini kwenye kikao hicho amesema hatua zimeanza kuchukuliwa tangu kuundwa kwa serikali ya mpito mwezi Aprili mwaka huu ikiwemo kufungulia mashtaka askari wa SPLA waliobainika kukiuka haki za binadamu na kupora mali za wananchi.

Ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchagiza usaidizi wa kibinadamu ambao Sudan Kusini inahitaji haraka.