Tume ya Uchunguzi yataka Eritrea ipelekwe mbele ya ICC

Tume ya Uchunguzi yataka Eritrea ipelekwe mbele ya ICC

Mwenyekiti wa tume ya uchunguzi ya haki za binadamu nchini Ertirea ameisihi Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kufungua kesi dhidi ya serikali ya Eritrea akisema kwamba kinachoendelea nchini humo tangu 1991 ni uhalifu dhidi ya ubinadamu. Ameongeza kwamba vitendo hivyo ni miongoni mwa kampeni ya kimkakati ya kudhibiti raia na kuendeleza utawala wa uongozi nchini humo.

Bwana Smith ametaja vitendo vyote vilivyoripotiwa na tume hiyo, ikiwa ni pamoja na mateso, ubakaji na utumwa. Ameongeza kwamba uhalifu huo unatekelezwa na serikali, viongozi wa chama tawala na jeshi la kitaifa, akisikitishwa kwamba serikali haina uwezo wa kitaasisi wala utashi wa kisiasa wa kufuatilia kesi hizo.

Pamoja na kupeleka kesi mbele ya ICC, Tume ya uchunguzi imependekeza kuweka vizuizi dhidi ya watu wanaoshakiwa kuwa wametekeleza uhalifu huo.

Hatimaye, Bwana Smith amesema, licha ya serikali ya Eritrea kuanza kuonyesha nia nzuri ya kuleta mabadiliko, bado hakuna katiba, bunge wala uhuru wa vyombo vya habari nchini humo, na bado watu wanateswa na kutishiwa na serikali na hivyo raia wa Eritrea hawawezi kufurahia haki zao.