Skip to main content

Rais Sassou Nguesso na mjumbe wa UM watoa wito kwa amani kwenye maziwa makuu

Rais Sassou Nguesso na mjumbe wa UM watoa wito kwa amani kwenye maziwa makuu

Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Ukanda wa maziwa Makuu Said Djinnit amekutana na Rais wa Jamhuri ya Congo Denis Sassou Nguesso ili kujadili masuala ya amani na usalama kwenye ukanda huo.

Taarifa iliyotolewa leo na ofisi ya Bwana Djinnit imeeleza kwamba mazungumzo kati yao yamefanyika baada ya kongamano la kimataifa la ukanda wa maziwa makuu (ICGLR) lililofanyika nchini Angola wiki iliyopita.

Bwana Djinnit amemfahamisha Rais Sassou Nguesso kuhusu mpango wa wawakilishi wa mkakati wa amani, usalama na ushirikiano kwa ajili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na ukanda wa Maziwa Makuu (PSC) wa kuongeza bidii katika kusalimisha vikundi vya watu waliojihami mashariki mwa DRC.

Wamejadili jinsi ya kutatua changamoto zilizopo katika kutekeleza huo mradi, huku Rais Sassou Nguesso akisisitiza umuhimu kwa viongozi wa ukanda huo kuendelea kujituma katika masuala ya amani, utulivu na maendeleo kwenye ukanda wa maziwa makuu.