Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waandamana Bahrain baada ya kiongozi wao kuvuliwa uraia

Waandamana Bahrain baada ya kiongozi wao kuvuliwa uraia

Nchini Bahrain maandamano makubwa yameripotiwa kwenye mji wa Diraz, kaskazini magharibi mwa nchi hiyo ambako ni makazi ya kiongozi wa kundi la madhehebu ya shia nchini humo, Sheikh Issa Qassem, kufuatia kitendo cha mamlaka nchi humo kumnyan’ganya uraia wake.

Ofisi ya haki za binadamu imesema kitendo hicho cha kuvuliwa uraia kwa kiongozi huyo ambaye ni mmoja wa watetezi wa haki za binadamu na wapinzani wa serikali kumefanya idadi ya watu waliopokwa uraia tangu mwezi Julai mwaka 2014 kufikia 250.

Ofisi hiyo imesema inatiwa hofu na mwendelezo wa msako dhidi ya watetezi wa haki na kusababisha hofu miongoni mwa jamii ikiwemo swala ya Ijumaa kusitishwa kwenye misikiti ya washia wakihofia usalama wao.

Ravina Shamdasani ni msemaji wa ofisi hiyo.

(Sauti ya Ravina)

“Tunasihi serikali ihakikishe wanaharakati hawakumbwi na shinikizo, vitisho au visasi kutokana na kazi na ushirikiano wao na vyombo vya haki vya Umoja wa Mataifa. Tunatoa wito kwa serikali kuchukua hatua za kujenga kuaminiana ikiwemo kuwaachia huru wale wote wanaoshikiliwa kwa kutetea haki za binadamu.”