Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mpango wa Kihistoria wa Utekelezaji kwa Albino barani Afrika waafikiwa

Mpango wa Kihistoria wa Utekelezaji kwa Albino barani Afrika waafikiwa

Kongamano la siku tatu la kikanda kwa ajili ya hatua kuhusu ulemavu wa ngozi barani Afrika limehitimishwa nchini Tanzania ambapo mpango wa kwanza kabisa wa utekelezaji umeanzishwa. Flora Nducha na maelezo zaidi.

Mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia 17-19 Juni uliandaliwa na Mtaalam Huru wa Umoja wa Mataifa, Ikponwosa Ero na washirika wake na kuhudhuriwa na washiriki 150 kutoka nchi 29 za kanda ya Afrika ikiwa ni pamoja na serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za kitaifa za haki za binadamu, wanaharakati, wataalam wa haki za binadamu kutoka Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika pamoja na wasomi.

Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa, nchini Tanzania Bw. Alvaro Rodriguez amesema, ‘usawa, utu na haki ndizo nguzo zinazopaswa kutuongoza katika mahusiano yetu na watu wenye ulemavu wa ngozi.

image
Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa, nchini Tanzania Bw. Alvaro Rodriguez.(Picha:UNIC/Tanzania/Stella Vuzo)
Mpango wa utekelezaji wa Mkutano huu wa kwanza katika Bara la Afrika unao uwezo wa kuifanya historia mateso na ukosefu wa usawa ambao watu wenye ulemavu wa ngozi hukumbana nayo.

Naye Bi Ikponwosa Ero amesema, “Kukiwa na wito mkubwa kutoka serikalini, ushirikiano kutoka kwa wadau wa maendeleo na ushirikishwaji wa mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali, tuna uhakika kutakuwa na mafanikio.”

image
Bi Ikponwosa Ero.(Picha:UNIC/Tanzania/Stella Vuzo)
Kwa nini Kongamano?

Kongamano hili limefanyika kwa sababu Mashambulizi dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi kwa ajili ya kuuza viungo vyao vya mwili yanaendelea kutokea katika bara la Afrika kutokana na ujinga kuhusu chanzo cha kisayansi cha ulemavu wa ngozi, vitendo vya ‘kishirikina’ na hatua zisizoridhisha za serikali. Ripoti ya vyama vya kiraia inaonesha kulikuwa na mashambulizi karibu 500 katika nchi 25. Haya ni matukio yaliyoripotiwa tu.

Matukio mengi hayaripotiwi kutokana na usiri katika masuala ya ushirikina, ushiriki wa familia, na uwezekano wa ushiriki wa matajiri na watu wenye nguvu,” alisema Ero. “

Hatua maalum zilizochukuliwa

Washiriki wa kongamano waliitikia wito na kutoa mapendekezo mazuri na kuandaa hatua maalum, rahisi na madhubuti ambazo zinaweza kutekelezwa na wadau wote. Hatua zilizochukuliwa zimewekwa katika maeneo manne: hatua za kuzuia, hatua za kulinda, hatua za uwajibikaji hatua za kupambana na ubaguzi.

image
Washiriki kutoka nchi mbali mbali ikiwemo viongozi katika jamii.(Picha:UNIC/Tanzania/Stella Vuzo)
Ahadi

Washiriki ikiwa ni pamoja na wawakilishi wa serikali waliahidi kutekeleza baadhi ya hatua hizo maalum kwa kufanya kazi na kulishughulikia suala hilo kitaifa, kutenga bajeti kwa ajili ya suala hilo na kuweka mtu au kamati ya kukabiliana na mgogoro huo katika kila eneo.

Washiraiki kutoka vyama vya kiraia waliahidi kuzishawishi serikali zao kufanya sensa ya uhakika ya watu wenye ulemavu wa ngozi na kupata taarifa zao ambazo ni muhimu kwa mipango sahihi na sera ya kukabiliana; kuhakikisha kuwa vifaa vya kuimarisha uwezo wa kuona vinapatikana kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa ngozi anapokuwa darasani na kutoa vizuia jua nafuu kama tiba muhimu ili kuzuia kansa ya ngozi, ambayo inaendelea kuondoa maisha ya maalbino.

image
Washiriki katika mkutano wa aina yake nchini Tanzania.(Picha:UNIC/Tanzania/Stella Vuzo)
Hatua zinazofuata

Mpango wa utekelezaji ulioandaliwa utachujwa na Mtaalam wa Umoja wa Mataifa kwa mwaka mmoja ujao na utakuwa kama kiwango cha bara zima cha kuwafanya wadau wote, hasa serikali, kuwajibika.

Kongamano limeandaliwa na Mtaalam Huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ulemavu wa Ngozi, Serikali ya Tanzania: Ofisi ya Waziri Mkuu, Timu ya Umoja wa Mataifa Tanzania, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania (“CHRAGG”), Benki ya Dunia, Sauti Zinazosimama, Under The Same Sun, Balozi za Norway, Ireland na Marekani nchini Tanzania, Ubalozi wa Canada nchini Tanzania.