Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa washikamana dhidi ya ukatili wa kingono vitani

Umoja wa Mataifa washikamana dhidi ya ukatili wa kingono vitani

Katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kupambana na ukatili wa kingono vitani, iliyokuwa Jumapili Juni 19, Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa katika suala hilo, Bi Zainab Bangura ameeleza kushikamana na wahanga wa ukatili wa kijinsia na familia zao nchini Iraq.

Akieleza kwamba ukatili wa kingono hutumiwa siku hizi si tu kama silaha ya vita, bali pia kama silaha ya ugaidi, bi Bangura amekariri kwamba huenda haki ikachelewa lakini haiwezi kunyimwa.

Bi Bangura ametuma ujumbe huo pamoja na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu nchini Iraq, Jan Kubis, akimulika madhara ya ukatili wa kingono kwa watu na jamii ya Iraq kwa ujumla ambayo inalengwa na kundi la kigaidi la ISIL.

Wamesema kwamba Umoja wa Mataifa utaendelea kuunga mkono jitihada za serikali ya Iraq katika kusaidia manusura, kuzuia na kupambana na uhalifu huo ambao hutokea kwa kiwango kikubwa nchini humo.