Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAMA yalaani mashambulizi Kabul na Badakhshan

UNAMA yalaani mashambulizi Kabul na Badakhshan

Mpango wa Umoja wa mataifa nchini Afghanistan (UNAMA) umeelezea hofu yake kuhusu mfululizo wa mashambulizi dhidi ya maeneo ya raia yaliyotokea leo, ambayo yamekatili maisha na kujeruhi wengine wengi.

UNAMA imesema moja ya mashambulio hayo limetokea katika maduka yenye watu wengi wilayani Kishem, jimbo la Badakhshan ambapo watu 10 wameuawa wakiwemo watoto na kujeruhi watu 36 wengi wao watoto.

Vilevile mapema leo asubuhi shambulio la Taliban la kujitoa muhanga limetokea kwenye umati wa watu mjini Kabul na kupoteza maisha ya watu 13 wahandisi wa ujenzi kutoka Nepal na kujeruhi wengine wanane wakiwemo walinzi wa wanadiplomasia wa Nepal na raia watatu wa Afghanistan.

UNAMA inasema kana kwamba hayo hayatoshi shambulio lingine likimlenga mjumbe wa serikali wa jimbo hilo Kabul limewajeruhi raia wanne akiwemo mjumbe huyo.

Talibani imedai kuhusika na mashambulio yote mawili ya Kabul ingawa imekanusha kuhusika na shambulio la Badakhshan.