Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika ni bara linalopokea wakimbizi zaidi

Afrika ni bara linalopokea wakimbizi zaidi

Idadi ya wakimbizi na wakimbizi wa ndani ikiwa imefika rekodi mpya katika historia, bara la Afrika limebainika kuwa bara linalopokea wakimbizi wengi zaidi duniani. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Hii ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR iliyotolewa leo, katika kuadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani.

Ripoti hiyo inaonyesha kwamba idadi ya wakimbizi na wakimbizi wa ndani ni zaidi ya milioni 65.3 mwaka 2015, ikilinganishwa na milioni 59.5 mwaka 2014.

Aidha UNHCR imesema kwamba nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara zimepokea wakimbizi milioni 4.4, ambapo Ethiopia, Kenya, Uganda, DRCongo na Chad zikiwa miongoni mwa nchi 10 zilizo karimu zaidi duniani.

Nusu ya wakimbizi wametoka nchi tatu ambazo ni Syria, Afghanistan na Somalia ambapo nusu yao ni watoto.

Ripoti hiyo mpya imeitia wasiwasi UNHCR, ikieleza kwamba mwelekeo huo ni hatari kwa usalama wa kimataifa, wakati ambapo mizozo mipya na ya muda mrefu inaendelea, huku katika ujumbe wake mkuu wa UNHCR Filippo Grandi akisema tatizo hilo ni ujumbe kwa jamii ya kimataifa.

(Sauti ya Bwana Grandi)

" Ujumbe wanaoleta ni kwamba, usipotatua matatizo, matatizo yatakufikia. Na huo ni ujumbe mzito, unaoumiza. Na unaumiz kwamba imechukua muda mrefu kwa watu wa nchi tajiri kuelewa ujumbe huo, lakini nadhani ni ujumbe wa kuchukua hatua.”