Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zeid ataka hatua dhidi ya ukiukwaji wa haki za WaRohingya, Myanmar

Zeid ataka hatua dhidi ya ukiukwaji wa haki za WaRohingya, Myanmar

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Zeid Ra’ad Al Hussein, ametoa wito kwa serikali mpya ya Myanmar ichukue hatua madhubuti ili kukomesha ubaguzi na ukiukwaji wa haki za vikundi vya walio wachache, hususan jamii ya Waislamu ya Rohingya katika jimbo la Rakhine.Maelezo zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Kamishna Zeid amesema hayo wakati akitoa ripoti mpya inayomulika hatma ya jamii za walio wachache nchini Myanmar.

Ripoti hiyo inaweka wazi aina mbalimbali za ukiukwaji wa haki za binadamu, ikionyesha kuwa jamii ya Rohingya inakumbwa ukiukwaji kama vile kupokonywa uraia kiholela, vikwazo vikali kwa uhuru wa kutembea, vitisho kwa maisha na usalama wao, kunyimwa haki za kupata huduma za afya na elimu, ajira za lazima, ukatili wa kongono, na kunyimwa haki za kisiasa.

Aidha, ripoti hiyo inasema kuwa mwelekeo wa ukiukwaji dhidi ya jamii ya Rohingya huenda ukawa ni uhalifu dhidi ya ubinadamu, ikitaka serikali ionyeshe azma ya kubadili mfumo wa sheria unaoruhusu ubaguzi na ukiukwaji huo.