Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Aibu ya waliobakwa iwageukie wabakaji:Ban

Aibu ya waliobakwa iwageukie wabakaji:Ban

Aibu wanayoihisi wahanga wa ubakaji na ukatili mwingine wa ngono wakati wa vita , ilelekezwe kwa watekelezaji wa uhalifu huo.

Huo ni ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon katika maadhyimisho haya ya kwanza kabisa ya siku ya kimataifa ya kutokomeza ukatili wa kingono katika vita ambayo inaadhimishwa leo Juni 19.

Ban ametoa wito wa kuendelea kuwasimamia wale wote ambao miili yao ilitumiwa kama silaha za vita, ingawa amesema kuna hatua kiasi zilizopigwa katika kushughulikia uhalifu huo.

Ameongeza kuwa ukatili wa ngono katika vita sasa unatambulika kila mahali kama ni mkakati wa kudhibiti, kuziogofya jamii na kuwalazimisha watu kuzikimbia nyumba zao.

Ban amesema “Uhalifu huo unaonekana kama ni tishio kwa amani na usalama wa kimataifa, ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu na pia ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo na maridhiano baada ya vita.

Hata hivyo Ban ametaja baadhi ya changamoto katika kushughulikia uhalifu huo ikiwa ni pamoja na makundi ya kigaidi kama Boko Haramu na Daesh ambayo yanaendelea kutumia ukatili wa ngono kuwavutia na kuendelea kumiliki wapiganaji na kujipatia mapato.

Nacho kitengo cha Umoja wa mataifa kinachohusika na masuala ya wanawake UN Women katika madhaadhimisho haya ya kwanza kimesema mwaka huu kimeshuhudia historia ya watu wengi kukutwa na hatia ya ukatili wa ngono walioutekeleza wakati wa vita Chad, Guatemala na Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR.

Kimeongeza kuwa kesi hizo ni ishara kwamba hatua zinachukuliwa kuhakikisha uwajibikaji wa vitendo hivyo vya kikatili.