Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutostahimili misimamo mikali kwadidimiza haki ya kukusanyika- Maina

Kutostahimili misimamo mikali kwadidimiza haki ya kukusanyika- Maina

Mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya uhuru wa kukusanyika kwa amani, amewasilisha ripoti yake mbele ya Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa inayoonyesha mvutano kati ya stahamala na kutostahimiliana kunakosababishwa na misimamo mikali.

Maina Kiai amewaambia wajumbe kuwa misimamo mikali si katika nyanja ya dini pekee bali pia katika harakati nyingine iwe soko huria, utamaduni au uzawa na kwamba misingi yake yote ni kanuni kali ambazo wahusika wanapaswa kuzingatia.

Amesema wakazi wa dunia wanazungumza lugha 7,000 dini kuu zikiwa 270 na wanaishi kwenye nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa wakiwa na maelfu ya utamaduni.

Maina amesema katika mazingira hayo ambamo kwayo sayari wanamoishi ni moja, dunia, ni lazima kustahimili tofauti za wengine licha ya kutokukubaliana katika baadhi ya masuala.

Amesema msingi wa stahamala ni uhuru wa kukusanyika ambao unatoa fursa kwa kila mkazi wa dunia kupaza sauti yake.

Hata hivyo amesema licha ya hali hiyo, serikali zinaelekea siko kwa kutunga sera au kuunga mkono mitazamo ya misimamo mikali inayodhibiti wenye hoja kinzani.