Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada ya shambulio la Orlando, Dieng aomba viongozi kutochochea hofu na chuki

Baada ya shambulio la Orlando, Dieng aomba viongozi kutochochea hofu na chuki

Mshauri Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari, Adama Dieng amesikitishwa sana na harakati za viongozi wa kisiasa na kidini kutumia shambulio la kigaidi la Orlando kama chanzo cha uchochezi wa chuki dhidi ya wapenzi wa jinsia moja na waislamu.

Kwenye taarifa iliyotolewa leo, Bwana Dieng amelaani shambulio hilo lililotokea kwenye klabu ya Pulse, mjini Orlando, Marekani na kusababisha vifo 49 pamoja na majeruhi 53.

Bwana Dieng ameeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu ongezeko la kauli za chuki na ubaguzi dhidi ya waislamu na wapenzi wa jinsia moja kufuatia shambulio hilo.

Amesema amefadhaishwa kusikia viongozi wa kidini wakikaribisha mauaji hayo, kutambua wahanga kama wapotovu, na kusihi serikali kuua wapenzi wa jinsia moja.

Aidha amehakiki baadhi ya viongozi wa kisiasa waliotambua waislamu wote kama wagaidi na kutaka wakatazwe Marekani.

Amesema vikundi vya walio wachache vinabaguliwa duniani kote, hata kwenye nchi zenye demokrasia, lakini hasa wakati wa matatizo kama hayo.