Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalam wa UM wataka hatua madhubuti kumaliza mzozo wa Burundi

Wataalam wa UM wataka hatua madhubuti kumaliza mzozo wa Burundi

Mwishoni mwa ziara yao ya pili nchini Burundi, wataalam watatu wa haki za binadamu wanaofanya uchunguzi huru kuhusu hali chini Burundi wametoa wito hatua madhubuti zichukuliwe ili kuumaliza mzozo uliopo nchini humo.

Christof Heyns, ambaye anaongoza timu ya wataalam hao watatu wa Umoja wa Mataifa, amesema moja ya vitu muhimu zaidi vilivyobadilika tangu mwanzoni mwa mwaka huu, ni kupungua kwa idadi ya mauaji ya watu.

Akikaribisha mabadiliko hayo, Bwana Heyns amesema wanakariri wito wao kwa pande zinazokinzana kukomesha matumizi ya ghasia kama nyenzo ya kisiasa.

Hata hivyo, mwenzie Pablo de Greiff ameonya kuwa hali iliyopo sasa ya angalau utulivu kidogo isidhaniwe kuwa ni ustawi wa muda mrefu, kwani bado kuna wasiwasi mkubwa kuhusu haki za binadamu, na hakuna ishara kwamba visa vya watu kutoweka na utesaji vimepungua. Aidha, amesema bado kuna ukwepaji sheria kwa ukiukwaji unaotendeka sasa na wa zamani.

Hali ya mashirika yasiyo ya kiserikali pia imemulikwa katika ziara hiyo, Bi Maya Sahli-Fadel, ambaye ni wa tatu katika timu hiyo akisema kwamba alishangazwa kuwa wawakilishi wote wa NGO waliokutana nao wakati wa ziara yao ya awali mwezi Machi, sasa wameikimbia Burundi.