Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kandanda huwaleta watu pamoja, yaweza kuendeleza amani- Kanu

Kandanda huwaleta watu pamoja, yaweza kuendeleza amani- Kanu

Je, wewe ni mkereketwa wa kandanda? Basi, utamkumbuka Nwankwo Kanu, nguli wa soka kutoka Nigeria- zamani akizichezea timu za Ajax, Inter Milan, na Arsenali.

Nyota huyo ambaye pia aliwahi kushinda medali ya dhahabu na timu ya Nigeria katika michuano ya Olimpiki, amesema mbali na furaha inayoibua katika wakereketwa wake, kandanda inaweza kutumiwa kuendeleza ulimwengu wenye amani zaidi.

Kanu, ambaye pia ni Balozi mwema wa Shirika la Kuhudumia Watoto (UNICEF), na Mwasisi wa Kanu Heart Foundation, amekuwa kwenye Umoja wa Mataifa kuhamasisha kuhusu mchango wa michezo katika kujenga amani na maendeleo.

Katika mahojiano na Redio ya Umoja wa Mataifa, ameeleza umuhimu wa kandanda na michezo kwa ujumla

“Inaleta furaha, na inaleta watu pamoja. Kwangu mie, naona ni chombo thabiti cha kuleta umoja na amani. Ni muhimu sana, kwani ili tuwe na ulimwengu bora, ni lazima kuwe na amani, ni lazima kuwe na umoja. Na watu wanapaswa kukumbuka kuwa elimu ni sehemu ya kandanda na sehemu ya michezo. Huwezi kutoa elimu bila michezo, na huwezi kufanya michezo bila elimu.”