Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa usawa miongoni mwa sababu za mauaji ya albino Afrika- Ero

Ukosefu wa usawa miongoni mwa sababu za mauaji ya albino Afrika- Ero

Kongamano la kwanza kabisa la kanda ya Afrika kuhusu hatua za kuchukua kulinda watu wenye ulemavu wa ngozi barani humo, Albino unaanza leo huko Dar es Salaam Tanzania ukiwa umeitishwa na Mtaalam huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu albino Ikponwosa Ero.

Akihojiwa na Stella Vuzo wa kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Bi. Ero amesema matarajio ni

(Sauti ya Bi. Ero)

“Kazi ya msingi itakuwa imewekwa kwa ajili ya hatua mahsusi zinazotekelezeka ili kuondokana na mapendekezo ya kufikirika ambayo mara nyingi ni vigumu kuyatafsiri mashinani na badala yake tuwe na hatua nyepesi na mahsusi ambazo watu wataweza kuzitekeleza kwenye nchi zao.”

Bi. Ero amesema kihistoria mauaji  ya albino yalichochewa pia na mila potofu lakini kwa sasa kwa mtazamo wake…

(Sauti ya Bi. Ero)

“Hali ngumu ya kiuchumi inachochea watu kutumbukiza mila potofu katika biashara.”

Zaidi ya washiriki 150 kutoka nchi 28 za Afrika wakiwemo viongozi wa serikali, wanasiasa na watalaamu wanatarajiwa kushiriki kongamano hilo huku Bi Ero akisema kuwa waganga wa jadi watajumuishwa katika mikutano ijayo baada ya utafiti ambao unafanyika kubaini tofauti kati ya ushirikina na tiba asilia.