Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchunguzi waendelea CAR kuhusu ukatili wa kingono licha ya mivutano

Uchunguzi waendelea CAR kuhusu ukatili wa kingono licha ya mivutano

Ofisi ya huduma za uangalizi wa ndani ya Umoja wa Mataifa OIOS inaendelea na uchunguzi kuhusu kesi za ukatili wa kingono zilizodaiwa kutekelezwa na walinda amani kwenye eneo la Kemo, nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema hayo leo akizungumza na waandishi wa habari akieleza kwamba uchunguzi huo unafanyika kwa pamoja na Burundi na Gabon.

Amesema tayari washtaki 90 miongoni mwa 106 wameshahojiwa na timu za pamoja, na pia:

(Sauti ya Bwana Dujarric)

“ Mashahidi wanahojiwa pia ili kuthibitisha shahidi. Utaratibu wa mahojiano unatarajiwa kutimizwa katika kipindi cha wiki chache zijazo. Madai hayo ni kuhusu vitendo vya mwaka 2014 na 2015 na kuna upungufu wa ushahidi wa kiafya na kisheria. Inamaanika kwamba kazi ya wachunguzi inategemea hasa ushahidi wa wahanga na mashahidi.”

Wakati huo huo, Bwana Dujarric ameeleza kwamba mivutano yanaendelea nchini CAR, mamia ya watu wakiwa wakisaka hifadhi kwenye kanisa katika maeneo ya Ouham-Pende kufuatia mashambulizi ya ex-Seleka, huku askari wa MINUSCA wakisambazwa kuhakikisha usalama wao.

Aidha ameongeza kwamba watu zaidi 1,300 wameripotiwa kukimbia CAR na kusaka hifadhi kwenye vijiji vilivyo mpakani mwa Cameroon na Chad, wakiwemo watoto 900, katika kipindi cha siku chache zilizopita. Tathmini ya mashirika ya Umoja wa Mataifa imeshabaini mahitaji yao ya dharura, wakati ambapo kukiwa na hofu ya kuongezeka kwa idadi ya wakimbizi kwenye eneo hilo kutokana na machafuko yanayoendelea.