Umoja wa Mataifa wachangia dola milioni moja kwa mazungumzo ya Burundi
Mfuko wa Ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa PBF umetangaza kuchangia dola milioni moja kwa Ofisi ya Mshauri Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini humo Jamal Benomar, ambayo jukumu lake ni kusaidia kutafuta suluhu ya amani kwa mzozo wa Burundi.
Kwenye taarifa iliyotolewa leo, Bwana Benomar amekaribisha ufadhili huo akisema umefika muda muafaka ili kuunga mkono jitihada za kuhamasisha mazungumzo thabiti na jumuishi, ambayo kwa mujibu wake ni ufunguo wa kutatua mzozo wa Burundi.
Aidha amesema lengo ni kuzalisha mazingira yatakayorahisisha mchakato wa amani.
Umoja wa Mataifa umepewa mamlaka ya kusaidia mazungumzo ya Burundi kupitia usaidizi wa kitaaluma kwa upatanishi unaoongozwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki.