Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban ahofia mkwamo wa kisiasa Haiti

Ban ahofia mkwamo wa kisiasa Haiti

Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon amesema anatiwa hofu na kuendelea kwa mkwamo wa kisiasa na hali ya sintofahamu nchini Haiti.

Ban anatambua kwamba hali ya sasa inaongeza changamoto za kisiasa na kijamii kwa kisiwa hicho, na kusema kuendelea na sintofahamu ya kisiasa na kuchelewesha zaidi mchakato wa uchaguzi kuna uwezekano wa kupindua hali ya utulivu iliyopo Haiti pamoja na msaada wa kimataifa kwa Haiti.

Katibu Mkuu ametoa wito kwa bunge la kitaifa kufanya maamuzi haraka kubaini mpango maalumu kwa serikali ya mpito kuhakikisha kwamba mchakato wa uchaguzi unakamilika na utawala wa katiba unarejea bila kuchelewa zaidi.

Ametoa wito kwa wadau wote kuwajibika ipasavyo kwa maslahi ya taifa na watu wake, ikiwa ni pamoja na kujizuia na vitendo vyovyote vitakavyochochea ghasia.