Wapinzani wabinywa Bahrain, Ban aingia hofu

16 Juni 2016

Nina wasiwasi kutokana na vitendo vya hivi karibuni vya mamlaka nchini Bahrain vya kudhibiti upinzani wa kisiasa nchini humo, amesema katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake.

Ban ametaja vitendo hivyo vya karibuni ikiwemo kuvunjwa kwa kikundi kikubwa cha upinzani wa kisiasa nchini Bahrain, Al Wefaq, sambamba na kukamatwa tena kwa mtetezi wa haki za binadamu Nabil Rajab.

Jambo lingine kwa mujibu wa msemaji huyo Stephane Dujarric ambalo linamtia wasiwasi Ban ni watetezi wa haki za binadamu kunyang’anywa uraia wao wanapotekeleza shughuli zao za utetezi wa haki pamoja na kukusanyika.

“Katibu Mkuu ana wasiwasi kubwa vitendo vya sasa dhidi ya upinzani vinadidimiza marekebisho yaliyofanywa na Mfalme Hamad ibn Isa Al Khalifa na vile vile kupunguza matumaini  ya kuwepo kwa mjadala shirikishi wa kitaifa kwa maslahi ya wakazi wote wa nchi hiyo ya kifalme.”

Katibu Mkuu amesema anashawishika kuwa utekelezaji thabiti wa mapendekezo kadhaa ikiwemo yale ya tume huru ya uchunguzi ya Bahrain kutatoa fursa ya kuimarisha hali ya haki za binadamu nchini humo pamoja na kushughulikia hofu ya raia.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter