Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kasi ya Boko Haram imedhibitiwa lakini bado changamoto- UNOCA

Kasi ya Boko Haram imedhibitiwa lakini bado changamoto- UNOCA

Jitihada za nchi za bonde la mto Chad zimesaidia kupunguza kasi ya mashambulizi ya mara kwa mara ya kikundi cha kigaidi cha Boko Haram kama ilivyokuwa awali.

Hiyo ni kwa mujibu wa Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa kwenye ukanda wa Afrika ya kati, UNOCA, Abdoulaye Bathily wakati akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani siku ya Jumatano.

Bathily amesema operesheni za mara kwa mara zinazofanywa na kikosi cha pamoja cha nchi hizo zimewezesha kukamatwa kwa wapiganaji wa Boko Haram, kuachiliwa huru kwa mateka na hata kurejesha maeneo yanayoshikiliwa na magaidi hao.

Hata hivyo amesema bado kuna changamoto kwa kuwa tathmini imebaini kuwa watendaji wa Boko Haram wanaishi na raia na hivyo kuendelea kuwa tishio kwa usalama wa kikanda..

“Kwa sababu hizo, ni muhimu kwa wadau wa kimataifa kuendelea na usaidizi wao kwa ukanda huu ili hatimaye kuondokana na vitisho vitokanavyo na Boko Haram. Halikadhalika kuendelea kusisitiza umuhimu wa hatua za kikanda kama ilivyosisitizwa kwenye mkutaon wa pili wa usalama wa kikanda uliofanyika tarehe 14 Mei huko Abuja. Naisihi jamii ya kimataifa kusaidia kikosi cha pamoja cha mataifa hayo kupitia usaidizi wa uhamasishaji wa kisiasa, vifaa na kifedha kulingana na mazingira.”

Nchi za Bonde la mto Chad ni pamoja na  Cameroon, Niger, Nigeria na Chad.