Skip to main content

Tuache kunyanyasa wazee- Ban

Tuache kunyanyasa wazee- Ban

Kuachana na tabia ya kuwapuuza, kuwanyanyasa na kuwasababishia ghasia wazee ni muhimu ili kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Hiyo ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon aliyotoa leo ikiwa ni sikku ya kimataifa ya kuhamasisha jamii kuachana na tabia za kuwatesa wazee.

Ban amesema ajenda 2030 inalenga kutokomeza umaskini na kujenga jamii endelevu kwa watu wote na hivyo ni muhimu kundi hilo nalo kujumuishwa ili kufanikisha malengo yote 17.

Vitendo vya kunyanyasa wazee vinafanyika kwa njia kadhaa ikiwemo kupigwa na wapenzi wao au wageni sambamba na kutumikishwa bila ujira.

Shirika la afya ulimwenguni linasema vitendo hivyo vinasababisha athari za kisaikolojia na karibu asilimia 10 ya wazee duniani wanakumbwa na athari hizo huku wanawake wazee wakiwa hatarini zaidi.

Kutokana na hali hiyo Katibu Mkuu ametaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kiraia kuazimia kuongeza maradufu jitihada zao kutokomeza unyanyasaji dhidi ya wazee.