Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haki ya barubaru kupata huduma ya afya izingatiwe- Mtaalam

Haki ya barubaru kupata huduma ya afya izingatiwe- Mtaalam

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya afya, Dainius Pûras, amezitaka nchi kuondoa vizuizi vyote vya kisheria vinavyosababisha vijana barubaru kushindwa kwenda kwenye vituo vya afya kusaka huduma, halikadhalika kusikilizwa na kunyimwa kufanya maamuzi yanayowahusu. Taarifa zaidi na John Kibego.

(Taarifa ya Kibego)

Baada ya kuwasilisha ripoti yake mbele ya  Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, Mtaalam huyo amezitaka serikali kuhakikisha kwamba haki za vijana barubaru zinalindwa hasa afya ya akili,  haki ya afya ya uzazi na udhibiti wa madawa kwa kuzingatia changamoto zitokanazo na masuala hayo.

Bwana Pûras amesisitiza kwamba ni lazima huduma za afya ziheshimu faragha, zizingatie matakwa mbalimbali ya kitamaduni, matarajio na maadili.

Aidha, alizitaka nchi zitunge au zijumuishe sera kamili ya haki ya afya ya uzazi katika mikakati ya kitaifa ili kuhakikisha haki ya masuala ya huduma na afya ya uzazi inafikiwa na wote.